Kenya-Uchaguzi 2013

Mahakama nchini Kenya yasema haiwezi kuwazuia Uhuru na Ruto kuwania urais

Mahakama Kuu nchini Kenya imesema haina mamlaka ya kuwazuia Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta na William Ruto kugombea urais nchini humo mwezi ujao.

Matangazo ya kibiashara

Wanaharakati nchini humo walifika Mahakamani kuitaka kuwazuia wawili hao kwa madai kuwa hawana maadili mema ya uongozi kwa mujibu wa katiba ya  nchini hiyo.

Uhuru na Ruto ambao ni washtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC kwa tuhma za kuchochea na kufadhili machafuko nchini humo mwaka 2007,  sasa watawania nyadhifa hizo za juu bila ya kuwepo kwa kizuizi chochote.

Majaji katika Mahakama hiyo ya Nairobi wamesema kuwa uamuzi wa kuamua ikiwa wawili hao hawana maadili mema ya kuwania nyadhifa hizo inaweza tu kuamuliwa na Mahakama ya Rufaa.

Aidha, Mahakama imeeleza kuwa kwa sasa ni vigumu kuwazuia wanasiasa hao kutogombea kwa sababu tayari Tume huru ya uchaguzi imekwisha wasafisha tayari kwa uchaguzi huo.

Wanaharakati nchini humo walitaka Mahakama kuwazuia wawili wao kwa kile walichoksiema kuwa wana kesi ya kujibu katika Mahakama ya ICC na hivyo hawana maadili mema kwa mujibu wa katiba ya Kenya na watashindwa kuiongoza Kenya ikiwa wataibuka washindi.

Wachambuzi wa siasa nchini humo wanasema kuwa uamuzi wa Mahakama ulitarajiwa na si wakuwashangaza hata kidogo kwa kile wanachosema kesi hiyo ilikuwa imeingizwa siasa.

Uchaguzi Mkuu nchini Kenya utafanyika tarehe 4 mwezi wa Machi huku ushindani mkubwa ukiwa kati ya Waziri Mkuu Raila Odinga na Naibu wake Uhuru Kenyatta.