MALI

Uchaguzi wa urais nchini Mali kufanyika tarehe 7 Julai

Uchaguzi wa urais nchini Mali utafanyika tarehe 7 mwezi wa Julai mwaka huu kwa mujibu wa serikali ya mpito nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Moussa Sinko Coulibaly Waziri wa Mambo ya ndani nchini humo amesema kuwa uchaguzi huo utasaidia kuweka uthabiti wa uongozi na usalama Kaskazini mwa nchi hiyo kutokana na oparesheni inayoongozwa na wanajeshi wa Ufaransa kuwasaka waasi wa Kiislamu.

Baada ya uchaguzi huo wa urais, uchaguzi wa wabunge utafanyika tarehe 21 mwezi huo wa Julai ukifuatiwa na duru ya pili ya urais ikiwa itakuwepo.

Uchaguzi ulitarajiwa kufanyika mwezi Aprili lakini kwa sababu ya maswala ya kiusalama haikuwezekana.

Mwezi uliopita, rais wa mpito wa Mali Dioncounda Traore alisema kuwa alitarajia kuwa uchaguzi huo utafanyika tarehe 31 mwezi wa Julai.

Wanajeshi wa Ufaransa wapatao elfu 4 wanaongoza vikosi vingine vya Afrika kupambana na waasi wa kiislamu Kaskazini mwa nchi hiyo.

Ufaransa imesema itaanza kuondoka nchini humo mwezi ujao na inataka Baraza la Usalama la Umoja kutuma jeshi la Kimataifa kulinda amani Kaskazini mwa nchi hiyo.