TUNISIA

Kiongozi wa Chama Cha Ennahda Ghannouchi kukutana na Rais Marzouki kusaka Waziri Mkuu Mpya wa Tunisia

Waziri Mkuu wa Tunisia Hamadi Jebali akitangaza kujiuzulu wadhifa wake kupitia Televisheni
Waziri Mkuu wa Tunisia Hamadi Jebali akitangaza kujiuzulu wadhifa wake kupitia Televisheni REUTERS/Zoubeir Souissi

Kiongozi wa Chama Cha Ennahda Rached Ghannouchi amesema baadaye hii leo atakutana na Rais Moncef Marzouki kujadili nani ambaye anafaa kuchukua wadhifa huo wa kuongoza serikali na kuendelea sera zao.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano Viongozi hao wenye ushawishi mkubwa kwa sasa kwenye siasa za Tunisia unakuja baada ya Waziri Mkuu Hamadi Jebali kutangaza kujizulu baada ya kushindwa kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa na kumaliza machafuko.

Ghannouchi na Rais Marzouki watakutana faragha kwa ajili ya kuangalia kiongozi ambaye anafaa kuchukua wadhifa wa kuongoza shughuli za serikali kipindi hiki ambacho mivutano nayo imeendelea kushuhudiwa.

Waziri Mkuu wa Jebali ametangaza kujiuzulu wadhifa wake kutokana na kile ambacho ameeleza ni kushindwa kwake kuunda serikali ambayo haiegemi mrengo wa kidini ili kumaliza machafuko nchini humo.

Tayari majina mawili yameanza kutajwa kurithi wadhifa wa Jebali mwenye umri wa miaka 63 akiwemo Waziri wa Afya Abdelatif Mekki na Waziri wa Sheria Moureddine Bhiri ambao wanaonekana wanaushawishi mkubwa.

Jebali amewasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Rais Moncef Marzouki akieleza anechukua hatua hiyo baada ya kushinda kufikia malengo ya kumaliza ghasia ambazo zimekuwa zikichangia na uwepo wa serikali inayoongozwa kwa misingi ya Kiislam.

Kiongozi huyo amesema anajiuzulu kama Mkuu wa Serikali kutokana na kushindwa kutimiza malengo yake sababu Taifa la Tunisia limeendelea kushuhudia machafuko kwenye maeneo mbalimbali.

Jebali amehutubia kupitia Televisheni na kusema lengo lake la kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa limeshindwa na ndiyo maana ameamua kujiweka kando na kupisha Kiongozi mwingine aongoze serikali.

Uamuzi wa Jebali kutangaza kujiuzulu umechochewa zaidi na upinzani ambao alikutana nao siku ya jumatatu ndani ya Chama chake cha Ennahda ambacho kinapinga hatua ya kuwepo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Jebali amesema amekatisha tamaa sana na msimamo wa Chama Cha Ennahda kwani kimekubali kuendelea kuona wananchi wa Tunisia wagawanyike katika misingi ya kisiasa kitu ambacho kimechangia machafuko.

Mwanasiasa huyo amesema hawezi akarejea kwenye serikali ya Rais Marzouki hadi pale ambapo kutakuwa kumetangazwa tarehe ya uchaguzi mkuu pamoja na kuanza kwa mchakato wa kupata katiba mpya.