SOMALIA

Mahakama ya Rufaa nchini Somalia kusikiliza rufaa ya kesi ya Mwandishi wa Habari Ibrahim juma lijalo

Mahakama ya Rufaa nchini Somalia imeanza kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mwandishi wa Habari Abdiaziz Abdinur Ibrahim aliyehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la kumhoji mwanamke aliyedai kubakwa na maofisa wa Polisi.

Waandishi wa Habari nchini Somalia wakifanya maandamano kushinikiza kuachiwa kwa mwandishi mwenzao Abdiaziz Abdinur Ibrahim
Waandishi wa Habari nchini Somalia wakifanya maandamano kushinikiza kuachiwa kwa mwandishi mwenzao Abdiaziz Abdinur Ibrahim
Matangazo ya kibiashara

Mwandishi Ibrahim alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja pamoja na mwanamke aliyejitangaza kubakwa kwa kosa la kuandika taarifa za uongo kwa mujibu wa serikali ambayo ilipinga kutokea kwa tukio hilo.

Mahakama ya Rufaa imeanza kusikiliza rufaa hiyo chini ya Jaji Hassan Mohamed Ali ambapo mahakama hiyo imeomba muda zaidi ili kuweza kupitia kwa umakini ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo.

Kesi hiyo kwa mujibu wa Jaji Ali inatarajiwa kuanza kusikilizwa juma lijalo baada ya taarifa zote muhimu na ushahidi kupitiwa na Mahakama ya Rufaa ikiwa ni pamoja na kupitia hukumu ya wali.

Ibrahim na mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 27 walihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kila moja kutokana na serikali kuwatuhumu kuitukana na kutaka kuwachafua maofisa wa Jeshi la Polisi.

Mwanasheria wa Ibrahim, Mohamed Mohamud Afrah amesema wamewasilisha ushahidi wao uliopokelewa na Mahakama ya Rufaa na wanasubiri kuanza kusikilizwa kwa rufaa yao hapo juma lijalo.

Afrah amesema wameiomba Mahakama ya Rufaa kuruhusu mashahidi ambao hawakupata nafasi ya kuhojiwa hapo awali wasikilizwe ili kujulikana ukweli wa tukio zima na hata Ibrahim kufikia hatua ya kumhoji mwanamke huyo.

Makundi ya Kutetea haki za Binadamu pamoja na Shirika la Human Rights Watch lenye makao yake nchini Marekani kwa pamoja yameilaani hukumu iliyokuwa imetolewa na kusema ni ya kisiasa zaidi.

Ibrahim kwa sasa anaendelea kutumikia adhabu hiyo ya kifungo cha mwaka mmoja huku mwanamke ambaye alijitangaza kubakwa na maofisa ya usalama akisubiriwa kuanza adhabu yake baada ya kumaliza kunyonyesha.