TUNISIA

Chama Cha Ennahda champendekeza Waziri wa Mambo ya Ndani Ali Larayedh kuwa Waziri Mkuu wa Tunisia

Waziri Mkuu Mteule wa Tunisia Ali Larayedh aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani tangu mwaka 2011
Waziri Mkuu Mteule wa Tunisia Ali Larayedh aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani tangu mwaka 2011 AFP / FETHI BELAID

Chama Tawala nchini Tunisia Cha Ennahda kimpendekeza jina la Waziri wa Mambo ya Ndani Ali Larayedh kuwania nafasi ya Uwaziri Mkuu nchini humo kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Waziri Mkuu aliyejiuzulu Hamadi Jebali. Tangazao la kupendekezwa kwa Waziri Larayedh kuwania nafasi ya Uwaziri Mkuu limetolewa na Mouadh Ghannouchi ambaye ni Mtoto wa Rais wa Chama Cha Ennahda Rached Ghannouchi.

Matangazo ya kibiashara

Chama Cha Ennahda kimempendekeza Larayedh kuwania nafasi hiyo ya Uwaziri Mkuu ili kumaliza hali ya sintofahamu iliyozuka nchini Tunisia na kuchangia kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Jebali.

Rais Moncef Marzouki anakutana na Kiongozi wa Chama Cha Ennahda Ghannouchi na Larayedh kwa ajili ya mazungumzo kabla ya kuchaguliwa rasmi kushika wadhifa huko wa kuongoza serikali.

Uteuzi huu unakuja baada ya hapo jumatano Rais Marzouki kutangaza Chama Cha Ennahda ndicho chenye haki ya kuteuwa Waziri Mkuu kutokana na kuwa na wabunge wengi na hivyo wanapata nafasi hiyo.

Rais Marzouki anatarajiwa kumpa kazi Waziri huyo wa zamani wa mambo ya Ndani Larayedh kuunda serikali mpya ili iendelee kufanyakazi ya kuwatumikia wananchi wa Tunisia.

Waziri Mkuu Mteule Larayedh anasiku kumi na tano za kuunda serikali mpya punde tu atakapotangazwa rasmi kuchukua wadhifa huo na kisha kuwasilisha majina hayo Bunge kwa ajili ya kuidhinishwa.

Larayedh amechukua wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Ndani tangu mwaka 2011 baada ya kuangushwa na Utawala wa Rais Zine El Abidine Ben Ali ambaye alimfunga na kumtesa Waziri Mkuu huyo Mteule.

Waziri Mkuu Jebali alijiuzulu wadhifa wake siku ya jumanne juma hili baada ya mpango wake wa kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa kugonga mwamba ndani ya Chama chake cha Ennahda.

Jebali aliamua kuunda serikali mpya baada ya kuzuka kwa maandamano kufuatia kuuawa kwa Kiongozi wa Upinzani Chokri Belaid aliyepigwa risasi na hivyo kuamsha hasira za wananchi wanaoukosoa Utawala wa Chama Cha Ennahda kinachoongozwa kwa kufuata misingi ya kiislam.

Taarifa za awali zilieleza Waziri wa Mambo ya Ndani larayedh alishateuliwa na Rais Marzouki na kisha kuidhinishwa na Baraza la Shura huku Mawaziri wengine waliokuwa wanatajwa kuchukua nafasi hiyo ni pamoja na Waziri Kilimo Mohamed Ben Salem, Waziri wa Sheria Noureddine Bhiri na Waziri wa Afya Abdellatif Mekki.