Zimbabwe

Mahakama kuu nchini Zimbabwe imetupilia mbali ombi la Wanaharakati kuwapa muda zaidi kabla ya kupiga kura ya maoni kupata Katiba mpya

Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe
Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe Reuters/Philimon Bulawayo

Mahakama Kuu nchini Zimbabwe imekataa kusikiliza ombi kutoka kwa kundi la wanaharakati wanaopinga Rasimu ya Katiba mpya kutaka katiba hiyo mpya isipigiwe kura mwezi huu.

Matangazo ya kibiashara

Wanaharakati hao wametaka Raia wa Zimbabwe wapewe muda zaidi kusoma Rasimu hiyo ya katiba na kuwa Majuma manne yaliyotolewa hayatoshi halikadhalika wamedai kuwa Raia hawakushirikishwa katika Mchakato wa Mabadiliko hayo.

Mahakama hiyo imesema haina uwezo wa kubadilisha tarehe ya kupigia kura rasimu hiyo na mabadiliko hayo yanaweza kufanywa tu na rais Robert Mugabe.

Baada ya zoezi hilo la kupigia kura ya maoni katiba mpya mwezi huu uchaguzi Mkuu unatarajiwa kufanyika mwezi Julai ambapo rais Robert Mugabe anatarajiwa tena kuwania tena urais.

Katiba mpya ni mabadiliko makubwa kuelekea katika uchaguzi Mkuu ili kupata mrithi wa Serikali ya Umoja iliyoundwa kati Rais wa nchi hiyo Robert Mugabe na Waziri Mkuu , Morgan Tsvangirai.