MALI

UNESCO kupeleka tume ya tathimini nchini Mali hivi karibuni

Irina Bokova, Mkurugenzi UNESCO
Irina Bokova, Mkurugenzi UNESCO blogunesco.blogspot.com

Shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia elimu, sayansi na utamaduni UNESCO limesema kuwa lipo tayari kupeleka kikosi chake nchini Mali hivi karibuni, kutathimini uharibifu uliofanywa dhidi ya vivutio vya asili. 

Matangazo ya kibiashara

Mkurugenzi wa UNESCO Irina Bokova akiwa katika ziara kwenye makao makuu ya umoja wa mataifa huko New York ameelezea mpango huo wa UNESCO mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa tayari wameanza mazungumzo na wafadhili wao ili kufanikisha mpango huo.

Bokova ameonya kuwa kumbukumbu za kale kutoka Timbuktu ziko katika hatari ya kusafirishwa nje ya Mali na ameahidi kusaidia kurejesha urithi wa mji huo ulioharibiwa na Waislam wenye msimamo mkali.

Waasi wanaohusishwa na kundi la kigaidi la Al-Qaeda walidhibiti mji wa Timbuktu mwaka jana na kusababisha kilio cha dunia kwa kuharibu makaburi ya kale ya Waislamu watakatifu ambayo wao wanayachukulia kama sanamu na kuchoma moto miswada isiyokadirika, kabla majeshi ya Ufaransa kuongoza kampeni ya kijeshi iliyofanikisha kuwaondoa katika miji muhimu mnamo Januari 28.