DRC

Watu wawili wapoteza maisha nchini DRC kwenye mapigano kati ya M23 na FDLR

REUTERS/James Akena

Hofu imeripotiwa kutanda katika mji wa Kiwanja mtaani Rutshuru mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC baada ya kutokea mapigano baina ya wapiganaji wa kundi la waasi la M23 na waasi wa Rwanda kutoka kundi la FDLR usiku wa kuamkia alhamisi hii ambapo watu wawili wamepoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa vibaya.

Matangazo ya kibiashara

Vyanzo vya serikali vimesema wapiganaji wa FDLR walifika katika duka moja kwa lengo la kuendesha uporaji na wapiganaji wa M23 walipopata taarifa walifika katika eneo hilo na kuanza kuwafyatulia risasi.

Hayo yanajiri wakati huu ambapo katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-Moon ametoa wito kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha mpango wa dharura wa kupeleka kikosi cha kimataifa cha kulinda amani katika eneo la mashariki mwa DRC kukabiliana na makundi yenye silaha ambayo yamekuwa yakidhorotesha usalama katika eneo hilo.

Vyama vya upinzani nchini humo vimepinga wito huo na kusema kuwa kupelekwa kwa kikosi hicho haina maana kwani itakuwa ni kuongeza idadi ya majeshi yasiyowajibika katika kuleta amani ya eneo hilo.