UFARANSA-MALI

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa kukutana na vikosi vya nchi hiyo vilivyoweka kambi Mali

REUTERS/Joe Penney

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian anazuru nchini Mali alhamisi hii na anatarajia kukutana na vikosi vya Ufaransa vinavyopambana na wapiganaji wa kiislamu katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo. Le Drian pia anatarajia kutembelea mji mkuu Bamako na mji wa kaskazini mwa Gao.

Matangazo ya kibiashara

Wizara ya Ulinzi ya Ufaransa imesema Le Drian ziara hiyo itaanzia katika bonde la Amettetai katika milima ya Ifoghas eneo ambalo vikosi vya Ufaransa na vile vya Chad vimekuwa vikiwasaka waasi waliofurushwa toka miji muhimu ya kaskazini waliyokuwa wakiishikilia kwa miezi kadhaa.

Akihojiwa na kituo cha Televisheni cha nchini Ufaransa cha France 24, Le Drian amesema ziara hiyo pia ina lengo la kutoa heshima kwa wanajeshi wao waliopoteza maisha kishujaa katika mapambano hayo.

Ziara hiyo inakuja wakati Mwanajeshi wa nne wa ufaransa ameripotiwa kuuawa katika makabiliano makali ya risasi jumatano hii katika milima ya Ifoghas kwenye operesheni kali dhidi ya ngome ya magaidi.

Wanajeshi takribani elfu nne wa Ufaransa wameingia nchini Mali kushirikiana na wanajeshi wa Mali na vikosi vya Magharibi mwa Afrika kukabiliana na wapiganaji wa kiislamu wanokinzana na serikali ya mpito ya Mali.