TUNISIA

Serikali mpya ya Tunisia kutajwa hii leo

Serikali ya Muungano nchini Tunisia inatarajiwa kutajwa hii leo ili kumaliza mzozo wa kisiasa nchini humo. Waziri mkuu mteule Ali larayedh amesema kuwa vyama vya kisiasa vilifikia makubaliano juu ya mpango wa kisiasa kwa ajili ya Serikali mpya ambayo itatekeleza mambo muhimu yanayopewa kipaumbele nchini humo.

Reuters / Loos
Matangazo ya kibiashara

Larayedh amesema serikali yake itajikita katika utekelezaji wa sera na uwajibikaji kama ambavyo amekuwa akisisitiza Rais wa nchi hiyo Moncef Marzouki.

Larayedh aliteuliwa tarehe 22 mwezi februari mwaka huu kuongoza Serikali mpya akiziba pengo lililoachwa na Hamadi Jebali ambaye alijiuzulu wadhifa wa Uwaziri Mkuu baada ya mpango wake wa kuunda serikali mpya ya wataalamu kukwama.

Majuma mawili aliyopewa Waziri Mkuu Larayedh ya kuhakikisha anawasilisha majina ya watu watakaounda Serikali mpya yanakamilika usiku wa hii leo.

Tunisia imekosa utulivu kwa muda sasa tangu kushuhudiwa kwa mauaji ya kiongozi wa upinzani Chokri Belaid ambaye alikuwa ni mkosoaji mkubwa wa serikali iliyopo madarakani.