KENYA-UCHAGUZI

Utulivu watawala nchini Kenya wakati matokeo ya Urais yakisubiriwa kwa hamu kubwa

REUTERS/Thomas Mukoya

Hali ya utulivu imeendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini Kenya wakati huu ambapo Tume Huru ya Uchaguzi na Ukaguzi wa Mipaka IEBC inatarajiwa kutangaza matokeo ya mwisho ya kiti cha Urais wakati wowote hii leo ijumaa.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa toka nchini humo zinasema biashara zimeathirika kutokana na wananchi wengi kuendelea kusalia nyumbani wakisubiri kujua nani aliyeibuka kinara katika kinyang'anyiro hicho.

Hatu ya wananchi kuendelea kusalia majumbani imechangia kuzorotesha shughuli za kibiashara na hata uchumi kuanza kuonekana kuathirika kwa sababu hakuna mzunguko wa kutosha wa fedha.

Jana alhamisi mgombea mweza wa Waziri Mkuu Raila Odinga, ambaye ni Makamu wa Rais anayemaliza muda wake Kalonzo Musyoka alitoa wito kwa IEBC kusitisha zoezi la uhesabuji kura kutokana na wao kubaini kasoro katika baadhi ya maeneo.

Musyoka alisema wana uthibitisho kuwa kumekuwa na udanganyifu katika zoezi hilo kwani katika baadhi ya maeneo kura za jumla zimekuwa zikizidi idadi ya wapiga kura waliojisajili shutuma ambazo zilikanushwa na Mwenyekiti wa IEBC Ahmed Isack Hassan.

Kwa matokeo ya hivi sasa kumekuwa na mchuano mkali kati ya wagombea wawili wa kiti cha Urais ambapo mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa Jubilee Uhuru Kenyatta anaongoza akifuatiwa na Waziri Mkuu Raila Odinga ambaye ni mgombea wa muungano wa CORD.