MALI-UFARANSA

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa akutana na wanajeshi wa Ufaransa nchini Mali

REUTERS/Joe Penney

Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amefanya ziara nchini Mali alhamisi hii na kukutana na vikosi vya Ufaransa vinavyopambana na wapiganaji wa kiislamu katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo ambapo.

Matangazo ya kibiashara

Wizara ya ulinzi ya nchi hiyo imesema Le Drian alianzia ziara yake katika bonde la Amettetai katika milima ya Ifoghas eneo ambalo vikosi vya Ufaransa na Chad vimekuwa vikiwasaka waasi waliofurushwa toka miji muhimu ya kaskazini waliyokuwa wakiishikilia kwa miezi kadhaa.

Waziri huyo pia amekutana kwa mazungumzo na Raisi wa mpito wa Nchi hiyo Diocounda Traore.

Baada ya mazungumzo hayo alielekea katika mji wa Gao ambako alisema ziara yake ina lengo la kuwatia moyo wanajeshi wa Ufaransa walioko katika eneo hilo na kuwapongeza katika kipindi hiki ambapo mapigano dhidi ya wapiganaji wa kiislamu yanaingia katika awamu ya mwisho.

Ziara hiyo inakuja wakati Mwanajeshi wa nne wa ufaransa ameripotiwa kuuawa katika makabiliano makali ya risasi jumatano juma hili katika milima ya Ifoghas kwenye operesheni kali dhidi ya ngome ya magaidi.

Wanajeshi takribani elfu nne wa Ufaransa wameingia nchini Mali kushirikiana na wanajeshi wa Mali na vikosi vya Magharibi mwa Afrika kukabiliana na wapiganaji wa kiislamu wanaokinzana na serikali ya mpito ya Mali.