DRC

Makundi mawili ya M23 yaendeleza mapigano mashariki mwa DRC

REUTERS/James Akena

Mapigano makali yaliyoyahusisha makundi mawili ya M23 yameshuhudiwa kuendelea Jumapili hii katika mji wa Rugari huko mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC, wakati huo huo wananchi wengi wameripotiwa kujificha katika nyumba zao kwa muda wa siku mbili sasa.

Matangazo ya kibiashara

Wapiganaji kutoka pande zote wamekuwa wakitupiana lawama wakati bado kuna utata kuhusu taarifa za kutekwa kwa miji kadhaa.

Mkuu wa shirika la msalaba mwekundu katika eneo la Bukima amesema mapigano hayo yamesababisha maafa kwa watu wengi ambao itakuwa ni mapema sana kujua idadi kamili.

Kundi la Sultani Makenga limepiga kelele kuhusu mauaji yanayofanywa na Majeshi ya Jean Marie Runiga, huku kukiwa na taarifa za ukiukwaji mkubwa wa Haki za binadamu.

Muungano wa mashirika ya kiraia umeeleza kusikitishwa na hali ya mapigano hayo na kusema kuwa yataathiri uchumi wa miji ya Goma na Rutshuru kwa kuwa barabara kutoka eneo hilo hadi Butembo imefungwa kufuatia kukithiri kwa mapigano hayo.

Hayo yanajiri wakati mapigano mengine yakishuhudiwa baina ya vikosi vya jeshi la serikali na waasi wa kutoka nchini Uganda wa ADF-NALU katika maeneo ya Eringeti mtaani Beni.