DRC

Makundi mawili ya M23 yashutumiana kutokana na mapigano mashariki mwa DRC

Viongozi wa kundi la waasi lililogawanyika la M23 Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC wameendelea kutuhumiana kutokana na mapigano makali yaliyoshuhudiwa mwishoni mwa juma katika miji ya Rugari na Rumangambo Mashariki mwa DRC.

REUTERS/James Akena
Matangazo ya kibiashara

Kwa siku kadhaa sasa waasi wa Sultan Makenga wamekuwa wakikabiliana na wale wa Askofu Jean Marie Runinga ambaye aliachishwa kazi na Makenga juma moja lililopita.

Kundi la Makenga limepiga kelele kuhusu mauaji yanayofanywa na Majeshi ya Runiga, huku kukiwa na taarifa za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Wakati huo huo Jean Marie Runiga anayeongoza kundi la pili la waasi wa M 23 naye anamtuhumu Makenga kwa kuanza mapigano hayo na kusema kuwa mpinzani wake huyo anaungwa mkono na serikali ya Kinshasa.

Wapiganaji kutoka pande zote wamekuwa wakitupiana lawama wakati wananchi wengi wameripotiwa kuendelea kujificha katika nyumba zao.

Hali ya mapigano kati ya makundi mawili ya M23 huenda ikaathiri mchakato wa mazungumzo ya amani kati yao na serikali ya Kinshasa jijini Kampala nchini Uganda.