BURUNDI-UFARANSA

Makubaliano ya kuisaidia Burundi kiuchumi yasainiwa

Serikali ya Ufaransa na Burundi wamesaini mkataba wa pamoja wa kuisaidia serikali ya Burundi kiuchumi katika siku zijazo. Mkataba huu umeafikiwa wakati wa ziara ya Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza nchini Ufaransa ambapo kiongozi huyo amekutana na kufanya mashauriano na mwenyeji wake Rais Francois Hollande.

Reuters / Alessandro Di Meo
Matangazo ya kibiashara

Katika hatua nyingine serikali hizo mbili pia zimeafikiana kuimarisha zaidi uhusiano wao wa kidiplomasia.

Ziara ya Nkurunziza imekuja wakati mazungumzo ya kisiasa yaliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa UN yakiendelea nchini Burundi na wadau wa chama tawala na wale wa upinzani wakishiriki mkutano huo.

Baadhi ya viongozi wa upinzani waliokuwa uhamishoni wamerejea kushiriki mazungumzo hayo, miongoni mwao ni pamoja na Alexis Sinduhije kiongozi wa chama pinzani cha upinzani cha MSD ambaye alirejea hivi karibuni.

Mkutano huo unatarajia kuja na mkakati mpya utakaosalidia Taifa hilo katika mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa Taifa hilo unaotarajiwa kufanyika mwaka 2015.

Umoja wa Mataifa umepongeza juhudi zinazofanywa na wanasiasa nchini Burundi katika kuzungumza na kuweka sawa mikakati ya kisiasa nchini humo kabla ya uchaguzi huo.