Mgomo wa vyombo vya habari binafsi waanza nchini Mali
Vyombo vya habari vya binafsi nchini Mali vimeanza mgomo wa kutotoa taarifa kwa umma wakipinga kukamatwa kwa mhariri wa gazeti la Le Republicain juma lililopita ambaye alichapisha taarifa kuhusu mazingira mabaya yanayowakabili wanajeshi wanaopambana na makundi ya wapiganaji wa kiislamu katika eneo la kaskazini mwa nchi ya Mali.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Mhariri huyo Boukary Daou alikamatwa na polisi jumatano iliyopita baada ya kuchapisha barua toka kwa wanajeshi iliyowalaumu wakubwa wao kuishi vizuri katika mji mkuu Bamako wakati wenyewe wanataabika katika mstari wa mbele kwenye mapigano eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.
Waziri wa mawasiliano Manga Dembele amesema mhariri huyo alifanya makosa kuchapisha barua hiyo ya wazi kwa Rais kuhusu maswala ya kijeshi, ingawa bado hakuna tamko rasmi toka kwa serikali ya mpito ya Mali juu ya tukio hilo.
Chama cha watetezi wa haki za wanahabari cha CPJ kimelaani kukamatwa kwa mhariri huyo na kusema vyombo vya usalama vimekiuka sheria huku wakitoa wito kwa serikali kuhakikisha mhariri huyo anaachiwa.
Magazeti mbalimabli huchapishwa kila wiki lakini hakuna hata moja lililoonekana mtaani asubuhi ya jumanne hii.
Redio 16 za binafsi nazo hazijasikika hewani huku nyingine zikisalia kupiga muziki pekee.
Wakati wanahabari toka vyombo binafsi wakigoma kutoa taarifa kwa umma shirika la kutetea haki za binadamu la umoja wa mataifa limewashutumu wanajeshi wa Mali kwa kuendesha mashambulizi dhidi ya makundi ya raia wasiokuwa na hatia na kuitaka serikali ya Mali ichunguze ukiukwaji huo wa haki za binadamu unaotendeka katika ardhi yake.