TUNISIA

Wpinzani wapinga tarehe ya kura ya maoni ya katiba mpya Tunisia

Wabunge wa upinzani nchini Tunisia wamepinga tarehe iliyowasilishwa na serikali kuhusu kupigia kura rasimu ya katiba mpya na kisha kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu baada ya kupatikana kwa katiba hiyo mpya.

REUTERS/Anis Mili
Matangazo ya kibiashara

Zoezi la upigaji kura lilikwama siku ya jumatatu na wabunge wanatarajiwa kuendelea na mjadala mwingine jumanne hii kabla ya kupitisha tarehe 24 Aprili kama tarehe rasmi ya kupigia kura rasimu ya katiba na 27 Oktoba kama tarehe ya uchaguzi mkuu.

Wapinzani wanaendelea kupinga mkakati huo na kutaka zoezi hilo lifanyike mapema zaidi.

Mvutano huo unakuja wakati Waziri Mkuu mteule Ali Larayedh anakabiliwa na changamoto nyingi za kuhakikisha serikali yake inakubalika huku mwenyewe akisisitiza kuwa ni lazima uchaguzi ufanyike mwishoni mwa mwaka huu.

Miaka miwili imepita tangu kuangushwa kwa utawala wa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Zine El Abidine Ben Ali lakini bado siasa za nchi hiyo hazijatengamaa huku mivutano ikiendelea kushuhudiwa baina ya vyama vikuu vya kisisiasa.