Mahakama yaamuru IEBC na Safaricom kutoa stakabadhi zilizoombwa na muungano wa CORD
Mahakama kuu jijini Nairobi imeamua kuwa muungano wa kisiasa wa CORD upewe stakabadhi muhimu inazozidai kutoka kwa Tume Turu ya Uchaguzi na Ukaguzi wa Mipaka IEBC pamoja na kampuni ya simu ya safaricom. Hata hivyo Jaji wa mahakama hiyo Isaac Lenaola amewataka wahusika wote katika kesi hiyo kufika mbele ya mahakama ijumaa hii kwa Maelekezo zaidi.
Imechapishwa: Imehaririwa:
CORD waliwasilisha kesi katika mahakama hiyo baada ya IEBC na Safaricom kugoma kuwakabidhi nyaraka muhimu ambazo wanataka kuzitumia katika uwasilishaji wa rufaa ya kesi ya kupinga matokeo ya urais yaliyomtangaza kwa Uhuru Muigai Kenyatta kama Rais mteule wa Taifa hilo.
Kiongozi wa CORD Raila Odinga akiwa akizungumza na wafuasi wake katika eneo la Kibera jijini Nairobi amesema bado anaamini mahakama itatenda haki kwa Wakenya na kufutilia mbali ushindi wa Kenyatta.
Muda mfupi baada ya matokeo rasmi kutangazwa mwishoni mwa juma, Odinga alizungumza na wanahabari na kusema watakwenda mahakamani kupinga matokeo hayo kwani IEBC wamefanya makosa katika utendaji wake na wana uthibitisho wa udanganyifu uliofanywa katika baadhi ya maeneo.
CORD wanawakilishwa na Mawakili 10 katika kesi hiyo na mahakama hiyo ina muda wa siku 14 kisheria kusikiliza na kuamua kesi hiyo.
Endapo mahakama itathibitisha kulikuwa na dosari katika uchaguzi huo itatoa uamuzi wa uchaguzi mwingine kufanyika ndani ya siku sitini na endapo hakutakuwa na dosari yoyote basi Rais mteule Uhuru Kenyatta na Naibu wake Wiliam Ruto wataapishwa mwezi Aprili mwaka huu.