SUDAN-SUDAN KUSINI

Rais wa Sudan Omar Hassan Al Bashir kuzuru Juba

REUTERS

Rais wa Sudan Omar Hassan Al Bashir amekubali mwaliko wa Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kuzuru Juba siku moja baada ya viongozi hao kukubali kuanza biashara ya mafuta. Taarifa kutoka serilai ya Juba zimethibitisha kuwa Rais Kiir alimpigia simu Bashir na kumpatia mwaliko huo ingawa bado siku rasmi ya ziara hiyo haijawekwa wazi.

Matangazo ya kibiashara

Ziara ya Bashir mjini Juba itakuwa ni ya kwanza tangu kiongozi huyo alipohudhuria sherehe za uhuru julai 9 2011 kufuatia kura ya maoni iliyoamua Kusini ijitegemee baada ya miaka 22 ya machafuko.

Mikutano miwili ya mapema mwaka huu haikuzaa matunda, lakini mapema jumanne hii Sudan na Sudan Kusini waliafikiana kuweka ratiba ya utekelezaji wa kurasa 16 za makubaliano ya mwezi septemba mwaka jana.

Mpatanishi wa Umoja wa Afrika AU ambaye ni Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki alishuhudia kusainiwa makubaliano hayo jijini Addis Ababa Ethiopia nchini Ethiopia.

Muafaka kati ya viongozi hawa wawili unatajwa kuwa huenda ukawa chanzo cha kupunguza uhasama na hata kurahisisha utekelezaji wa makubaliano ya amani baina ya mataifa hayo mawili.

Mfululizo wa mashambulizi katika eneo la mipaka ya Sudan na Sudan Kusini ilizua hofu kuhusu uhusiano wa mataifa hayo jirani ambayo yalishindwa kutekeleza makubaliano yaliyosainiwa mwezi septemba.

Taarifa za hivi karibuni zinasema tayari Sudani Kusini imeondoa wanajeshi wake zaidi ya elfu hamsini kutoka katika mpaka wake na Sudani Kaskazini hatua ambyo imekuja siku moja baada ya kufikiwa kwa makubaliano ya kuanza uzalishaji na usafirishaji wa mafuta.