KENYA

Raila Odinga ataka muungano wa Jubilee uheshimu uamuzi utakaotolewa na Mahakama

Reuters / Luc Gnago

Waziri Mkuu wa Kenya anayemaliza muda wake Raila Amolo Odinga na kiongozi wa muungano wa kisiasa wa CORD ameutaka muungano wa Jubilee wa Rais mteule Uhuru Muigai Kenyatta kukubali uamuzi utakaotolewa na Mahakama ya rufaa kuhusu kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na Magavana, Maseneta na wabunge wa muungano wa CORD jijini Nairobi, Odinga amesema wana uhakika kuwa wataibuka na ushindi katika kesi yao kupitia mahakama.

Odinga pia amekashifu hatua ya Rais mteule kuanza kutekeleza majukumu ya kiserikali kwa kukutana na viongozi wa usalama na baadhi ya mabalozi wakati kesi kuhusu ushindi wake ikitarajiwa kuwasilishwa Mahakamani hapo kesho.

Odinga ameendelea kusistiza kuwa yeye ndiye aliyeshinda uchaguzi huo na zoezi la kuhesabu matokeo halikuwa huru.

Muungano wa CORD uliteua Mawakili wake kumi watakaosimamia kesi ya kupinga matokeo yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Ukaguzi wa Mipaka ya nchini Kenya IEBC na kusema wana ushahidi juu ya udanganyifu uliofanyika katika kura za wagombea wa nafasi ya Urais.

Ikiwa mahakama itabaini uchaguzi huo ulikuwa na dosari itaamuru kufanyika kwa uchaguzi mwingine na iwapo itabaini hakukuwa na dosari Rais mteule Uhuru Muigai Kenyatta na naibu wake William Rutto wataapishwa mwezi April.