DRC-M23

Wafuasi wa Sultani Makenga wapinga kutambuliwa kwa Jean Marie Runiga kama mwenyekiti wa M23

Kundi moja la waasi la M23 linaloegemea upande wa Sultan Makenga Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo DRC wamesema wameshangazwa na mpatanishi wa mazungumzo ya amani kati ya kundi hilo na serikali ya Kinshasa kusema anamtambua Jean-Marie Runiga kama mwenyekiti wa kundi hilo.

AFP PHOTO / Junior D.Kannah
Matangazo ya kibiashara

Kundi la M23 limegawanyika baada ya Sultan Makenga kumfuta kazi Runiga na kumteua Bertrand Bisimwa kama kiongozi mpya kwa madai kuwa Runiga anashirikiana na Bosco Ntaganda ambaye anatafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC.

Hata hivyo msemaji wa kundi la M23 linalongozwa na Bisimwa, Amani Kabasha amesema wataendelea na shughuli zao kama kawaida.

Mwishoni mwa juma lililopita mapigano makali kati ya makundi mawili ya M23 yalishuhudiwa katika miji ya Rugari na Rumangambo Mashariki mwa DRC na kusababisha wananchi wengi kujificha katika nyumba zao kwa zaidi ya siku mbili.

Mgawanyiko huo ulioshuhudiwa katika siku za hivi karibuni huenda ukaathiri muafaka uliotarajiwa katika mazungumzo ya amani ya jijini Kampala kati ya M23 na serikali ya Kinshasa.