KENYA

CORD kuwasilisha mahakamani kesi ya kupinga matokeo ya urais wa Kenya leo

Muungano wa kisiasa wa CORD unaongozwa na Waziri Mkuu wa Kenya Raila Amolo Odinga unatarajia kuwasilisha kesi katika Mahakama ya juu nchini humo kupinga ushindi wa Rais mteule wa Taifa hilo Uhuru Muigai Kenyatta. Awali Viongozi wa muungano huo walitarajiwa kuwasilisha kesi hiyo ijumaa lakini waliahirisha mpaka leo jumamosi ambapo ni siku ya mwisho ya uwasilishaji wa rufaa, kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

Waziri mkuu wa Kenya na mgombea wa muungano wa CORD Raila Odinga
Waziri mkuu wa Kenya na mgombea wa muungano wa CORD Raila Odinga rfi
Matangazo ya kibiashara

James Orengo ambaye amewahi kuwa waziri wa ardhi nchini Kenya aliwaambia waandishi wa habari kuwa bado wanaamini muungano wao wa CORD utaibuka na ushindi na kusema hawakupenda kuwasilisha kesi yao sambamba na mashirika mengine ambayo yaliwasilisha kesi yao katika mahakama hiyo siku ya ijumaa.

Siku ya jumatano CORD walikwenda mahakamani kudai haki yao baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Ukaguzi wa Mipaka IEBC na kampuni ya simu ya Safaricom kukataa kuwapatia baadhi ya stakabadhi walizokuwa wakihitaji katika uwasilishaji wa kesi yao.

Mahakama ilisikiliza pande zote na kisha kuamuru CORD wapewe stakabadhi hizo.

Hata hivyo bado muungano wa CORD unaituhumu IEBC kuendelea kuwasumbua kupata baadhi ya stakabadhi wanazohitaji licha ya mahakama kuamuru wapewe.

Baada ya kesi hiyo kuwakilishwa, mahakama itatoa siku tatu kwa washatakiwa yaani IEBC kupewa nyaraka za kuwataka kufika mahakamani ndani ya siku tatu ili kujibu mashtaka yanayowakabili.

Tayari muungano wa Jubilee na Mwanasheria Mkuu nao wameomba kujumuishwa katika kesi hiyo na mahakama inatarajiwa kutoa uamuzi ndani ya siku 14.

Ikiwa mahakama itabaini uchaguzi huo ulikuwa na dosari itaamuru kufanyika kwa uchaguzi mwingine na iwapo itabaini hakukuwa na dosari Rais mteule Uhuru Muigai Kenyatta na naibu wake William Rutto wataapishwa mwezi April mwaka huu.