ZIMBABWE

Wananchi wa Zimbabwe kupigia kura rasimu ya katiba mpya

Reuters

Wananchi wa Zimbabwe wanatarajia kupigia kura rasimu ya katiba mpya hatua ambayo inatajwa kutoa mwelekeo wa kuelekea uchauzi mkuu wa mwezi julai mwaka huu. Mamilioni ya wananchi wanatarajiwa kupiga kura hapo kesho jumamosi na asilimia kubwa wanatarajiwa kuunga mkono rasimu hiyo kufuatia kuwepo kwa kipengele kinachopunguza madaraka ya Rais pamoja na muda wa Rais kukaa madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Ni miaka 33 sasa tangu Rais wa nchi hiyo Robert Mugabe aingie madarakani, amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono mabadiliko ya katiba licha ya ukosolewaji anaoupata toka kwa jumuiya ya kimataifa kuhusu utawala wake.

Hata hivyo bado kuna hofu kubwa juu ya vyombo vya usalama, hivi karibuni Mkuu wa jeshi la Polisi Augustine Chichuri aliwaambia Maofisa wa polisi kuwa yeyote ambaye hataunga mkono chama tawala cha ZANU-PF hatakuwa na nafasi ya kuendelea kuwepo katika jeshi hilo.

Maofisa wa polisi katika maeneo yote ya nchi wametakiwa kujisajili kama wapiga kura na kukipigia kura chama tawala katika uchaguzi mkuu ujao.

Matukio kama haya bado yanazua hofu iwapo katiba mpya itakuwa na ukombozi wa kisiasa, kiuchumi na kifikra kwa wananchi wa Taifa hilo ambao wamekuwa chini ya Rais Mugabe na chama chake cha ZANU-PF kwa zaidi ya miongo mitatu.

Wanasiasa wa upinzani wamekuwa wakilalamikia hatua ya vyombo vya usalama kujihusisha na siasa na wanahofia huenda mustakabali wa siasa za nchi hiyo hususani katika uchaguzi wa mwezi julai ukawa sio wa kidemokrasia.