ALGERIA

Vijana wasiokuwa na ajira waandamana nchini Algeria

Maelfu ya vijana wa Algeria wasiokuwa na ajira wanaandamana kutaka mamlaka husika kuwapatia ajira za kudumu na kuondolewa kwa sheria zinazowakandamiza watu wasiokuwa na ajira. Waandamanaji hayo yamechochewa zaidi na wanaharakati wa kutetea haki za watu wasiokuwa na ajira kutoka maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ambao wamekuwa wakiikosoa serikali kutokana na kukosa mbinu mbadala za kukabiliana na tatizo hilo.

REUTERS/Stringer
Matangazo ya kibiashara

Vijana wanaokadiriwa kuwa ni zaidi ya elfu tatu wameonekana katika mitaa ya jiji la Algiers wakiwa na mabango yanayopeleka ujumbe kwa serikali kuwa wamechoshwa na ukosefu wa ajira unaowaandama.

Mwanaharakati wa watu wasiokuwa na ajira, Tarek Mameri ameelezea maandamano hayo kama ni mafanikio ya kwanza katika harakati zao za ukombozi.

Watu 15 walioshiriki mgomo uliopita katika mji wa Ouargla wanatarajiwa kufikishwa mahakamani tarehe 26 ya mwezi huu kujibu mashtaka ya kufanya kusanyiko kinyume na sheria.

Watu wengine wanne walihukumiwa kifungo cha mwezi mmoja na mahakama ya Laghouat baada ya kufanya maandamano haramu nje ya Shirika la Ajira la Taifa katikati ya mji mkuu wa Algeria.

Jumatatu hii Waziri Mkuu wa Algeria Abdelmalek Sellale alitoa wito kwa makampuni yaazoendesha shughuli zake nchini humo kuhakikisha raia wazawa wasiokuwa na ajira wanapewa kipaumbele kwenye ajira zinazotolewa nchini humo.

Algeria ina uhaba mkubwa wa ajira na asilimia 21.5 ya vijana wote wenye umri chini ya miaka 35 wanaishi katika mazingira duni kutokana na ukosefu wa ajira.