KENYA

Hatima ya kisiasa nchini Kenya ipo mikononi mwa Mahakama ya Juu

Kenya imeingia katika wiki ambayo wananchi wa taifa hilo wanasubiri uamuzi wa Mahakama ya Juu nchini humo ndani ya siku kumi na nne zijazo kuamua ikiwa ushindi wa rais mteule Uhuru Kenyatta ulikuwa halali au la.

Matangazo ya kibiashara

Jumamosi iliyopita, muungano wa kisiasa wa CORD unaongozwa na Waziri Mkuu Raila Odinga uliwasilisha kesi katika Mahakama hiyo kuitaka kutupilia mbali ushindi wa Uhuru Kenyatta kama rais mpya kama ilivyotangazwa na tume ya Uchaguzi nchini humo.

Muungano huo unasema kuwa una ushahidi wa kutosha kuonesha kuwa tume ya uchaguzi nchini humo IEBC ilihusika pakubwa na wizi wa kura kwa lengo la kumwangusha Odinga.

Waziri Mkuu Raila Odinga amesema kuwa uamuzi wake wa kwenda Mahakamani ni kutaka haki kufanyika na ukweli kubainika kuhusu mshindi halali wa uchaguzi huo, haki anayosema inaweza kutolewa tu na Mahakama hiyo ya Juu ambayo ni ya kwanza kabisa nchini humo.

Naye rais mteule Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wao wameendelea kuwaomba  wakenya kuungana pamoja na kuliombea taifa hilo wakati huu huku kila mmoja akisubiri uamuzi huo wa Mahakama.

Ikiwa Majaji wa Mahakama hayo wakiongozwa na Jaji Mkuu Willy Mutunga wataamua kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na haki rais mteule Uhuru Kenyatta ataapishwa baada ya wiki moja na ikiwa itabainika kuwa kulikuwa na dosari hiyo basi uchaguzi huo utarudiwa baada ya siku sitini.

Wachambuzi wa siasa nchini humo wanasema kuwa huu ni wakati wa Mahakama hiyo ya juu kuonesha uwezo wake  kutokana na uamuzi ambayo unasubiriwa si tu nchini Kenya bali pia katika Jumuiya ya Kimataifa.