Mawakili wa Uhuru Kenyatta waomba Majaji wa ICC kumwondolea mashtaka mteja wao
Mawakili wa rais mteule wa Kenya Uhuru Kenyatta wamewaomba Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya ICC kumwondelea Mashtaka yote yanayomkabili mteja wao ya kufadhili na kuchochea machafuko ya baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2007 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya elfu moja na maelfu kukimbia makwao.
Imechapishwa:
Wakiongozwa na Wakili Steven Kay, wamewataka Majaji wa Mahakama hiyo pia ikiwa hawataitupilia mbali kesi hiyo wairudishe katika Mahakama ya kuthibitisha ikiwa mteja wao ana kesi ya kujibu au la baada ya upande wa Mashtaka kumwondelea kesi Francis Muthaura ambaye pia alikuwa anatuhumiwa kushirikiana na Kenyatta.
Kay amesisitiza kuwa kuondolewa kwa Mashtaka dhidi ya Muthaura na pia kujiondoa kwa shahidi mkuu katika kesi hiyo inamaanisha kuwa haina uzito.
Ikiwa Majaji wa Mahakama hiyo wataamua kuendelea na kesi hiyo na ikiwa Uhuru ataapishwa kama rais wa Kenya basi atakuwa rais wa kwanza kwenda Hague kufunguliwa mashtaka yanayomkabili katika Mahakama hiyo ya Kimataifa.
Uhuru Kenyatta ameendelea kukanusha kuwa alipanga na kufadhili machafuko hayo kwa kuwalipa kundi la Mungiki kutekeleza mauaji dhidi ya wafuasi wa chama cha kisiasa cha ODM mjini Nakuru na Naivasha.
Hata hivyo, upande wa Mashtaka unaongozwa na Fatou Bensouda umeendelea kusisitiza kuwa una ushahidi wa kutosha dhidi ya Kenyatta na alihusika kwa njia ya kipekee kufadhili machafuko hayo.
Shahidi mwingine wa Naibu rais mteule William Ruto amejiondoa kushiriki katika kesi dhidi ya Ruto kwa madai kuwa alisema uongo dhidi ya mshtakiwa huyo ambaye pia anatuhumiwa kuchochea machafuko hayo.
Kesi dhidi ya Ruto na aliyekuwa Mtangazaji Joshua Arap Sang inatarajiwa kuanza mwezi wa tano huku, ile ya uhuru Kenyatta ikitarajiwa kuanza mwezi Julai.