Kenya-Uchaguzi 2013

Mahakama ya Juu nchini Kenya yaonya dhidi ya kesi ya kupinga matokeo ya urais kujadiliwa nje ya Mahakama

Mahakama ya Juu nchini Kenya inayosikiliza kesi iliyowasilishwa na muungamo wa kisiasa wa CORD unaongozwa na Waziri Mkuu Raila Odinga na Mashirika ya kijamii kupinga kutangazwa kwa Uhuru Kenyatta kama mshindi wa uchaguzi wa urais nchini humo imeonya dhidi ya kuzungumzia kesi hiyo nje ya Mahakama hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Mahakama hiyo Willy Mutunga amesema Mahakama hiyo inafahamu kwa undani kesi hiyo na inastahili tu kuzungumzwa ndani ya Mahakama hiyo.

Mutunga amewataka Mawikili wa walalamishi na washtakiwa kuwaeleza madhara yanayoweza kutokea ikiwa kesi itaanza kujadiliwa nje ya Mahakama hiyo.

Aidha, Mutunga ametoa wito kwa vyombo vya habari nchini humo kutoa habari zisizoegemea upande wowote kuhusu kesi hiyo inayoendelea katika Mahakama hiyo.

Muungano wa CORD unaituhumu Tume ya Uchaguzi nchini humo kwa kutoandaa uchaguzi huru na wa haki tarehe 4 mwezi wa Machi na pia ilichangia pakubwa kumsaidia Uhuru Kenyatta kutangazwa mshindi.

Waziri Mkuu Odinga ameendelea kusisitiza kuwa Mawakili wake wana ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa Tume hiyo ya Uchaguzi  IEBC haikuandaa uchaguzi uhuru na haki.

Uamuzi wa Mahakama hiyo ya Juu nchini humo utafanywa na Majaji sita wakiongozwa na Jaji Mkuu Willy Mutunga chini ya wiki mbili zijazo.

Ikiwa Mahakama itatupilia mbali kesi hiyo Uhuru Kenyatta ataapishwa baada ya siku saba kama rais wa nne wa Kenya na ikiwa itabainika kuwa kulikuwa na wizi wa kura basi Majaji wa Mahakama hiyo wataamuru kuwa uchaguzi huo urudiwe baada ya siku sitini.

Wakati uamuzi wa Mahakama ukisubiriwa vita vya maneno vinaendelea kati ya Waziri Mkuu Raila Odinga na rais mteule Uhuru Kenyatta.

Kenyatta anamtaka Odinga kuacha kuzungumzia namna uchaguzi ulivyokuwa na kusubiri uamuzi wa Mahakama jambo ambalo Odinga anasema hawezi kuacha kulizungumzia.

Aidha, Odinga amemtaka Kenyatta kuacha kutumia mali ya serikali kama vile magari ,ndege ya rais kwa kile anachokisema kuwa bado hajathibitsihwa kama rais wa Kenya.

Wakenya na dunia nzima inasubiri uamuzi wa Mahakama hiyo ya juu kuamua mustakabali wa kisiasa nchini humo.