UN-BANGUI

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lalaani shambulizi la waasi wa Seleka nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN limelaani vikali kitisho cha waasi wa Seleka nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambao wametishia kuanzisha mashambulizi upya dhidi ya serikali ya rais Francois Bozize.

Matangazo ya kibiashara

Baraza hilo pia limeshtumu shambulizi lililotekelezwa hivi karibuni na waasi hao wa Seleka katika mji wa Bangassou jambo wanalosema linaweza kuendelea kuhatarisha hali ya usalama nchini humo.

Kauli ya baraza la usalama inakuja wakati ambapo rais Bozize amelazimika kuwaachilia huru mateka wote wa kivita aliowakamata kufuatia shinikizo la waasi wa Seleka.

Waasi wa Seleka walianza mpango wa kuiangusha serikali ya rais Bozize mwezi Desemba mwaka uliopita baada ya kuituhumu serikali ya Bangui kushindwa kutekeleza ahadi walizoafikiana kuhusu uongozi wa nchi hiyo mwaka 2007.

Mwafaka uliotiwa saini mapema mwaka huu jijini  Gabon nchini Libreville, kiongozi wa upinzani nchini humo Nicolas Tiangaye ni Waziri Mkuu mpya na kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa wadhifa atakaoushikilia hadi mwaka ujao wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Mwishoni mwa Juma lililopita, waasi wa Seleka waliwakamata na kuwazuia Mawaziri watano wakiwemo wanachama wao kwa madai kuwa walishindwa kushinikiza serikali kuwaachia huru wafuasi wao.