MALI-UFARANSA

Marekani yaiorodhesha kundi la Ansar Dine kama kundi la kigaidi nchini Mali

Wanajeshi wa Ufaransa na Chad wameendelea na msako wao katika Milima ya Ifoghas karibu na mpaka wa Algeria kuwasaka waasi wa Kiislamu waliotekeleza shambulizi la bomu mjini Timbuktu na kusababisha kifo cha mwanajeshi wa Mali pamoja an waasi wengine.

Matangazo ya kibiashara

Wakati Oparesheni hiyo ikiendelea,  serikali ya Marekani imetangaza kujumuisha kundi moja la wapiganaji wa Kiislamu wa Kaskazini mwa Mali kwenye orodha ya makundi hatari kwa nchi hiyo.

Nchi hiyo imelitaja kundi la Ansar Dine lenye uhusiano wa karibu na mtandao wa Al-Qaeda kuwa la kigaidi kama kundi hatari kwa usalama wa Marekani na kuongeza kuwa itawasaka viongozi wake popote walipo.

Wakati Marekani ikitoa orodha hiyo hali ya usalama Kaskazini mwa Mali imeendelea kuimarika licha ya mapigano kuripotiwa huku wanajeshi wa Ufaransa wakitarajiwa kuondoka hivi karibuni.

Waziri wa mambo ya nje wa Chad, Moussa Faki Mahamat amesema licha ya wanajeshi wa Ufaransa kutarajiwa kuondoka nchini humo Umoja wa Afrika una vikosi imara kuchukua hatamu ya kulinda usalama wa Mali.

Serikali ya Ufaransa imesema kuwa itayaondoa majeshi yake nchini humo kuanzia mwezi ujao baada ya kumaliza Oparesheni yao na kuwaachia wanajeshi wa Afrika.

Tangu kuanza kwa oparesheni hiyo wanajeshi watano wa Ufaransa wamepoteza maisha yao huku wanjeshi 26 wa Chad wakiuawa.