Waasi wa Seleka wazidi kuukaribia mji mkuu wa Bangui nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati
Kundi la waasi la Seleka linalopambana na serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati limesema linakaribia kuingia katika mji mkuu wa nchi hiyo Bangui, wakati mapigano yakiendelea kushuhudiwa baada ya kukwama kwa utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya Seleka na serikali ya Bangui. Kiongozi mkuu wa waasi hao Colonel Djouma Narkoyo ameongea kwa njia ya simu na shirika la habari la AFP na kusema tayari wameshavuka mji wa Damara na wanatarajia kuingia Bangui hivi karibuni.
Imechapishwa:
Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa imethibitisha kuwa waasi hao wapo kilometa chache kutoka Bangui huku ikitoa wito kwa pande zinazokinzana kusitisha mapigano na kuheshimu haki za raia wanaotaabika kutokana na mapigano hayo.
Hata hivyo serikali ya Bangui kupitia radio ya Taifa imekanusha taarifa za waasi hao kuvuka mji wa Damara huku ikiwataka raia wake kutohofia taarifa hizo.
Wakati hali ikizidi kuchacha nchini Jamhuri ya Afrika ya kati, Rais wa nchi hiyo Francois Bozize amekutana na Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma kwa mazungumzo ijumaa hii, tovuti ya serikali imeeleza ingawa haijaweka wazi mazungumzo hayo yamejiegemeza katika swala lipi.
Waasi wa Seleka walitangaza kurejea katika makabiliano na wanajeshi wa serikali baada ya kudai makubaliano yaliyotiwa saini mjini Librevile nchini Gabon kati ya kundi hilo na serikali mapema mwaka huu hayajatekelezwa.