TANZANIA

Idadi ya watu waliopoteza maisha nchini Tanzania kufuatia kuanguka kwa Jengo la Ghorofa 16 imefikia 34

Jengo la Ghorofa 16 lililoporomoka Jiji Dar Es Salaam nchini Tanzania limesababisha vifo vya watu 34 hadi sasa
Jengo la Ghorofa 16 lililoporomoka Jiji Dar Es Salaam nchini Tanzania limesababisha vifo vya watu 34 hadi sasa Kwa hisani ya Ikulu ya Tanzania

Idadi ya watu waliopoteza maisha nchini Tanzania katika Jiji la Dar Es Salaam imefikia 34 kipindi hiki Kikosi Maalum Cha Uokozi kikiendelea na zoezi la kuondoa kifusi ili kuangalia kama kuna miili zaidi imenasa chini ya mabaki ya jengo lenye ghorofa 16.

Matangazo ya kibiashara

Zoezi la kusaka miili ya watu walionaswa kwenye malundo ya vifusi limeendelea kwa siku tatu mfululizo usiku na mchana ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Saidi Mecky Sadick amethibitisha wameshapata miili ya watu 34.

Miili kumi imepatikana kuanzia siku ya jumapili hadi mapema asubuhi ya leo ambapo Kikosi hicho kikitumia zana mbalimbali kimeendelea kuhakikisha kinaondoa kifusi na kufika chini ambako kuna ghorofa tatu.

Mkuu wa Mkoa wa Jiji la Dar Es Salaam amesema Kikosi kinaendelea na kazi ya kuondoa kifusi huku akiwa na matumaini huenda wakakuta miili zaidi ikiwa chini kwani kwa siku tatu ni ngumu kukuta mtu akiwa hai.

Miongoni mwa wale ambao wamepoteza maisha ni watoto wawili ambao wanatajwa kufikwa na mauti wakiwa wanacheza chini ya Jengo hilo la ghorofa kumi na sita ambalo lilikuwa linaendelea kujengwa.

Watu kumi na wanane ndiyo walitoka wakiwa salama baada ya kuokoleewa saa kadhaa baada ya kuporomoka kwa jengo hilo la ghorofa huku wanne kati yao wakiendelea kupatiwa matibabu katika Hospital ya Muhimbili kitengo cha Mifupa MOI.

Makadirio ya awali yameonesha kati ya watu 60 hadi 70 walikuwepo eneo hilo wakati jengo hilo linaporomoka siku ya Ijumaa na tayari watu wanane wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wakihusishwa na kuanguka kwa ghorofa hilo.

Lengo hilo lilikuwa mali ya Shirika la Nyumba la Taifa NHC na Shirila la Ujenzi la Ladha na hatari jeshi la Polisi linaendelea kuwahoji watu wanane ambao wanatajwa kuhusika kwenye uzembe uliochangia kuanguka kwa jengo hilo la ghorofa 16.