SUDAN

Serikali ya Sudan imewaachia huru wafungwa sita wa kwanza wa kisiasa waliokuwa wanashikiliwa katika Gereza la Kober

Wafungwa wa Kisiasa wakiachiwa nchini Sudan baada ya kushikiliwa katika Gereza la Kober
Wafungwa wa Kisiasa wakiachiwa nchini Sudan baada ya kushikiliwa katika Gereza la Kober

Mamlaka nchini Sudan imewaachia wafungwa sita wa kisiasa waliokuwa wanashikiliwa katika gereza la Kober ikiwa ni mwanzo wa utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais Omar Hassan Al Bashir alilolitoea wakati akifungua vikao vya Bunge. Wafungwa hao sita wameachiwa kwa msamaha wa Rais Al Bashir na wamekuwa wakishikiliwa kwenye gereza la Kober lililopo Kaskazini mwa Khartoum kwa kipindi tofauti.

Matangazo ya kibiashara

Miongoni mwa wale wafungwa wakwanza wa kisiasa walioachiwa nchini Sudan ni pamoja na Hisham Mufti na Abdul Aziz Khalid ambao wote ni wafuasi wa upinzani waliokuwa wanashikiliwa kwa kipindi cha miezi mitatu.

Wafungwa hao wa kisiasa wamepokelewa kwa furaha na ndugu na jamaa zao ambao walikuwa nje ya gereza hilo wakipongeza hatua ya Rais Al Bashir kutangaza mpango wa kuwaachia wafungwa wa kisiasa.

Wanasiasa wengi ambao wanashikiliwa nchini Sudan ni pamoja na wale ambao walishiriki kwenye mkutano uliofanyika mwezi januari nchini Uganda wakiatajwa kupanga njama za kuiangusha serikali.

Kiongozi wa Muungano wa Vyama vya Upinzani zaidi ya 20 nchini Sudan Farouk Abu Issa ameshindwa kuchangia lolote baada ya kuachiwa kwa wafungwa hao sita wa kisiasa licha ya hapo jana kusema kauli ya Rais Al Bashir haiaminiki.

Mtaalam Huru kutoka Umoja wa Mataifa UN Mashood Adebayo Baderin amesema wafungwa wote wa kisiasa wanapaswa kuachiwa nchini Sudan ili kuhakikisha kuna kuwa na utengamano.

Baderin amesema Viongozi wa Upinzani na hata raia wa kawaida ambao wanashikiliwa kwa makosa ya kusingiziwa wanapaswa kuachwa huru ili kuhakikisha usalama wa taifa unaimarishwa.

Rais Al Bashir siku ya jumatatu alitangaza serikali yake itawaachia wafungwa wote wa kisiasa na kuwa tayari kufanya mazungumzo na Wapinzani ili kuondoa matatizo ya kisiasa ambayo yameota mizizi.