JAMHURI YA AFRIKA YA KATI-UGANDA

Uganda yasitisha kwa muda msako dhidi ya Kiongozi wa Kundi la Waasi la LRA Joseph Kony anayejificha Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Kiongozi wa Kundi la Waasi la LRA Joseph Kony anayesakwa na Majeshi ya Uganda
Kiongozi wa Kundi la Waasi la LRA Joseph Kony anayesakwa na Majeshi ya Uganda

Serikali ya Uganda imetangaza kusitisha zoezi la kumsaka Kiongozi wa Kundi la Waasi la LRA Joseph Kony ambaye anatajwa kujificha nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati na kufanya mashambulizi katika taifa hilo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Sudan. Jeshi nchini Uganda kupitia Msemaji wake Felix Kulayigye ndilo limetangaza kusitishwa kwa msako huo wa Kiongozi wa LRA Kony kwa muda hadi pale ambapo maelezo zaidi yatatolewa.

Matangazo ya kibiashara

Kulayigye amesema hawataondoa wanajeshi wao waliopo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati lakini kwa sasa kuna mambo ambayo yanafanyiwa kazi kwanza kabla ya operesheni ya kumsaka Kony kuendelea.

Msemaji wa Jeshi la Uganda amesema wamelazimika kusitisha opersheni hiyo kutokana na nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa sasa kuwa chini ya Utawala Mpya baada ya kuangushwa kwa serikali ya Francois Bozize.

Kulayigye ameongeza kuwa msako huo umesitishwa kutokana na Utawala wa sasa chini ya Muungano wa Seleka kutotambuliwa na Umoja wa Afrika AU na ndiyo maana hata wao hawawezi kuendelea na shughuli zao kama awali.

Uganda ina maelfu ya wanajeshi wake nchini Jamhuri ya Afrika ya kati ambao walipelekwa ikiwa ni sehemu ya mapngo wa kumsaka Kony pamoja na kundi lake kutokana na kuwa kitisho cha usalama huko Kampala.

Kiongozi wa Kundi la Waasi la LRA Kony anahofiwa kujificha pamoja na kundi lake katika misitu ambayo inapatikana katika mpaka wa nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na mataifa ya Sudan na Sudan Kusini.

Kony anatuhumiwa kuwaajii watoto kwenye jeshi lake pamoja na kuendesha vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa wanawake na katika kipindi cha miaka 25 ambayo amekuwa na Kundi la LRA.