SUDANI-SUDANI KUSINI

Sudani yaahidi kuboresha uhusiano wa kidiplomasia na Sudan Kusini

Rais wa Sudani Omar Al Bashir amesema kuwa nchi yake itaimarisha uhusiano wa kidiplomasia na Sudani Kusini ikiwa ni pamoja na kurejesha uhusiano wa kibiashara katika hali yake ya kawaida.Bashir amesema ziara yake nchini Sudani Kusini ni ishara ya kuanza msingi wa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili na hivyo kumaliza matatizo na migogoro iliyodumu kwa kipindi kirefu. 

Matangazo ya kibiashara

Kwa upande wake Rais wa Sudani Kusini Salva Kiir amesema kuwa amekubaliana na Rais Al Bashir kuendelea kufanya mazungumzo ambayo yatasaidia kupata suluhu ya maswala yote yanayohusiana na mgogoro kati ya nchi hizo mbili jirani za Afrika.

Al Bashir aliwasili nchini Sudan Kusini hii leo na kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Sudan Salva Kiir katika uwanja wa ndege wa Juba.

Miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele katika mazungumzo ya viongozi hao ni swala la usalama ambalo limekuwa tete tangu nchi hizo zigawanyike mwezi Julai mwaka 2011.

Muafaka kati ya viongozi hawa wawili unatajwa kama chanzo cha kupunguza uhasama na hata kurahisisha utekelezaji wa makubaliano ya amani baina ya mataifa hayo.

Mpango wa Al Bashir kuzuru Juba uliwekwa wazi siku moja tu baada ya viongozi wa mataifa haya mawili ya Sudan kuafikiana kuanza upya biashara ya uzalishaji na usafirishaji wa mafuta.

Ziara ya Bashir mjini Juba inakuwa ni ya kwanza tangu kiongozi huyo alipohudhuria sherehe za uhuru Julai 9 2011 kufuatia kura ya maoni iliyoamua Kusini ijitegemee baada ya miaka 22 ya machafuko.