DRCONGO-M23-MONUSCO

Waasi wa M23 wasema watajibu mashambulizi endapo watavamiwa na vikosi vya UN

REUTERS/James Akena

Kundi la wapiganaji waasi wa M23 wanaokinzana na serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC wameonya kuwa watajibu mashambulizi endapo watavamiwa na vikosi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa UN. Msemaji wa M23 Vianey Kazarama ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kundi lao halina haki ya kuwavamia walinda amani hao lakini endapo watachokozwa watatumia uwezo wao kupambana na vikosi hivyo.

Matangazo ya kibiashara

Kauli hiyo toka kwa waasi wa M23 imekuja baada ya vikosi vya UN vinavyolinda amani nchini jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUSCO kusema kwamba haivitishwi na tambo za kichochezi zinazotolewa dhidi yao na waasi wa M23.

Aidha waasi hao wamekua wakitoa vitisho kwa majeshi ya Tanzania, Malawi na Afrika Kusini yanayotarajiwa kuwa sehemu ya kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa UN kitachokuwa na jukumu la kupambana na makundi ya waasi wanaoyumbisha usalama wa DRCongo.

Mwezi uliopita baraza la usalama la umoja wa mataifa UNSC lilipitisha azimio la kuundwa kwa kikosi hicho cha wanajeshi 2500 watakaokabiliana na makundi ya uasi katika eneo lenye mgogoro mashariki mwa DR Congo.

Waasi wa mashariki mwa DRC wamekuwa wakipinga uamuzi wa uvamizi wa kijeshi dhidi yao badala yake wanadai UN ilipaswa kuunga mkono jitihada za upatikanaji wa suluhu ya kisiasa ili kupata amani ya kudumu katika eneo hilo.