MISRI

Mahakama nchini Misri yaamuru kuachiliwa huru kwa Hosni Mubarak

Mahakama nchini Misri imeamuru kuachiliwa huru kwa rais wa zamani wa nchi hiyo Hosni Mubarak kuhusu mauaji ya waandamanaji mwaka 2011 ili kuanza upya kusikiliza kesi hiyo ya mauaji inayomkabili.

Matangazo ya kibiashara

Mamia ya waandamanaji waliuliwa kwa kupigwa risasi na polisi wakati wa maandamano ya kumwondoa uongozini Mubarak harakati walizofaulu kwa kuiangusha serikali hiyo.

Hata hivyo, Mubarak  ataendelea kuzuiliwa kusubiri kukamilika kwa  uchunguzi zaidi kuhusu tuhma za kuhusika na visa vya ufisadi na utumizi mbaya wa mamlaka alipokuwa uongozini.

Mahakama hiyo jijini Cairo ilitoa agizo hilo la kuachiliwa kwa Mubarak siku ya Jumatatu baada ya muda wake wa miaka miwili wa kuzuiliwa jela kukamilika.

Wakili wa Mubarak  aliomba Mahakama jijini Cairo kumwachilia huru mteja wake baada ya kuzuiliwa kwa kipindi hicho chote licha ya kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

Mwezi Januari mwaka huu, Mahakama ilikubali ombi la kuachiliwa huru kwa Mubarak kuhusu kifungo cha maisha jela wakati huu anapokabiliwa na mashtaka mengine mapya ya ufisadi pamoja na wanawe Alaa na Gamal ambao pia wanazuiliwa.