Zambia

Rais wa zamani wa Zambia Rupiah Banda akamatwa tena

Rais wa zamani wa Zambia Rupiah Banda alikamatwa tena siku ya Jumatatu na kuachiliwa huru kwa dhamana baada ya kutuhumiwa kuhusika na kashfa ya ufisadi kuhusu ununuzi wa Malori tisa ya kumfanyia kampeni za kisiasa mwaka 2011.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa tume ya kumchunguza rais Banda Namukolo Kasumpa amesema kuwa tayari Banda amehojiwa kuhusu tuhma hizo kuhusu Lori anazodaiwa kuwa alizipata kwa njia isiyo halali kutoka kwa kampuni moja ya ujenzi nchini humo.

Banda mwenye umri wa miaka 76 ambaye alihudumu kama rais wa nchi hiyo kati ya mwaka 2008 na 2011 aliondolewa na bunge haki ya kumlinda kama rais mstaafu na kufunguliwa makosa kadhaa ya ufisadi.

Banda sasa anatarajiwa kufikishwa Mahakamani tarehe 30 mwezi huu kujibu tuhma hizo za ufisadi zinazomkabili.

Rais huyo wa zamani wiki iliyopita pia alihojiwa kuhusu uamuzi wake wa kuuza shamba kwa mwekezaji mmoja kutoka nchini Misri kinyume na sheria ya nchi hiyo.

Wiki iliyopita rais Banda alizuuliwa katika uwanja wa ndege mjini Lusaka kuondoka nchini humo kushuhudia kuapishwa kwa rais mpya wa Kenya Uhuru Kenyatta jijini Nairobi.

Banda na wanasiasa wa upinzani wanadai kuwa mbinu za kumshtaki rais huyo wa zamani ni za kisiasa na kujaribu kuudhoofisha upinzani.