KENYA

Serikali ya Kenya yawaagiza Mabalozi wake wote duniani kurejea nyumbani

Serikali ya Kenya imewaagiza Mabalozi wake wote 52 wanaowakilisha nchi hiyo katika mataifa mbalimbali duniani kurudi nyumbani ndani ya kipindi cha wiki moja.

Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa Utumishi wa Umma Francis Kimemia amesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kutokana na hatua ya serikali mpya ya Nairobi kuwa na mpango mpya kuhusu  sera zake za mambo ya nje na mahitaji ya katiba mpya.

Katiba mpya nchini humo inasema kuwa ni sharti Mabalozi wote wanaoteuliwa na rais wachunguzwe na kupitsihwa na bunge kabla ya kutumwa katika mataifa mbalimbali duniani kinyume na ilivyokuwa zamani ambapo rais aliwateau tu Mabalozi bila ya kuchunguzwa.

Wakati hayo yakijiri, rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Wiliam Ruto wanatarajiwa kutangaza baraza jipya la Mawaziri wiki hii na duru zinasema baraza hilo litakuwa na Mawaziri 18.

Siku ya Jumanne, rais Kenyatta atalihutubia bunge la Kitaifa na lile la Senate kutoa sera za serikali yake  kwa wabunge na Maseneta waliochaguliwa wakati wa uchaguzi Mkuu uliopita.

Mwishoni mwa juma lililopita, rais Kenyatta alikutana na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga na Makamu wa rais Kalonzo Musyoka katika Ikulu ya Nairobi kujadili namna ya kuimarisha umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi huo kuligawa taifa hilo.

Odinga anayeongoza muungano wa siasa wa CORD amewaambia wafusi wake kuwa wao kama upinzani watahakikisha kuwa serikali ya Kenyatta inatakeleza katiba mpya na kuikosoa bungeni.