DRC

Mswada wa kukosa imani na Waziri Mkuu wa DRC Matata Ponyo watupiliwa mbali

Bunge la Kitaifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limetupilia mbali mswada wa kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Matata Ponyo uliowasilishwa na upinzani nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Mswada huo ulitupiliwa mbali baada ya wabunge 42 kuondoa sahihi zao licha ya kuunga mkono na kusababisha kutupiliwa mbali kutokana na kukosa idadi inayohitajika kikatiba kwa mswada kama huo kujadiliwa bungeni.

Upinzani nchini DRC kupitia Mbunge Baldwin Mayo wa chama cha UNC aliwasilisha mswada huo baada ya awali wabunge 130 kuutia sahihi kuunga mkono mswada huo.

Katiba nchini humo inasema kuwa mswada kama huo unaweza kujadiliwa na kupitishwa ikiwa wabunge 125 kati ya 500 watauunga mkono mswada huo.

Wabunge wa upinzani wamewashtumu wenzao kutoka upande wa serikali kwa kujiondoa katika daikika za lala salama kabla ya mswada huo kuwasilishwa bungeni kwa kile wanachosema ni kinyume na sheria za bunge na katiba.

Kabla ya mswada huo kutupiliwa mbali, wafuasi wa chama tawala cha MP waliandamana  jijini Kinsasha kumuunga mkono Waziri Mkuu Ponyo kwa madai kuwa serikali yake imejitahidi kuunda nafasi zaidi za kazi.

Wakati mswada huo ukitupiliwa mbali waakazi wa mji wa Goma na maeneo mengine Mashariki mwa nchi hiyo wameendelea kuishi kwa hofu ya kuvamiwa na makundi ya waasi wakati huu wajumbe wa serikali wakiendelea na mazungumzo na viongozi wa waasi wa M 23 jijini Kampala Uganda.