SUDAN KUSINI

Rais wa Sudan Kusini Salva Kirr apunguza mamlaka ya makamu wake

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir ametoa agizo la kupunguza mamlaka ya naibu wake Riek Machar hatua ambayo huenda ikasababisha machafuko ya kikabila nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hiyo ya rais Kiir inaamanisha kuwa Machar ambaye ni mpiganaji wa zamani wa msituni na anayefahamika kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya kabila la Nuer sasa atahusika tu na kazi aliyopangiwa kikatiba nchini humo, lakini haikufahamika wazi ni mamlaka yepi hayo yaliondolewa.

Kuanzia siku ya Jumanne, jukumu kubwa la Machar litakuwa ni kumwakilisha rais Kirr wakati anapokuwa nje ya nchi hiyo kuwa mwanachama wa baraza la Mawaziri na baraza la Kitaifa la Usalama.

Uamuzi wa rais Kiir pia una maana kuwa hatua za Machar za kujaribu kuweka mipango ya kuliunganisha taifa hilo ambalo limekumbwa na ukabila huenda zikadidimia.

Kamati ya uwiano wa kitaifa nchini humo imevunjwa na rais Kiir suala ambalo raia nchini humo wamesema wameshangazwa na hatua hiyo ya rais.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa Machar ni mwanasiasa ambaye msimamo wake mara nyingi huwa haueleweki kutokana na wakati mmoja kuunga  na kutounga mkono kujitenga  kwa Sudan Kusini  wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1983 hadi 2005.

Wakati mmoja, wapiganaji wake wa SPLM kutoka kabila la Nuer walijitenga na kuunga mkono serikali ya Khartoum wakati wa mapambano ya kujitenga kwa Sudan Kusini huku vikosi vyake vikituhumiwa kuwaua watu wa kabila la Dinka katika mji wa Bor mwaka 1991.