KENYA-ICC

Ruto ataka Mahakama ya ICC kumruhusu kutohudhuria vikao vyote huko Hague

Naibu wa rais wa Kenya William Ruto ameiomba Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC kumruhusu kutohudhuria vikao vyote wakati kesi yake itakapoanza kusikilizwa mjini Hague nchini Uholanzi.

Matangazo ya kibiashara

Ruto anaitaka Mahakama hiyo kuwaruhusu mawakili wake kumwakilisha wakati wa kesi hiyo au kujiunga na Mahakama hiyo kupitia njia ya Video kutoka jijini Nairobi.

Hata hivyo, Ruto amesema kuwa atahudhuria vikao hivyo wakati wa ufunguzi na wakati wa kufunga kesi dhidi yake.

Wakili wa Ruto Karim Khan, ameongeza kuwa ikiwa ombi hilo litakubaliwa na Mahakama hiyo itakuwa imemtendea haki mteja wake.

Ruto anatuhumiwa na makosa ya ukiukwaji wa haki za ubinadamu ikiwemo mauaji na ubakaji visa vilivyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 tuhma ambazo Ruto ameendelea kuzikanusha.

Mbali na Ruto rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anatuhumiwa pia kufadhili na kuchochea machafuko hayo, naye ameiomba Mahakama hiyo kumruhusu kuhudhuria vikao hivyo kupitia video.

Ombi la rais Kenyatta hata hivyo lilikataliwa na Mahakama hiyo kwa kile ilichosema kuwa itaigharimu fedha nyingi kuweka mitambo hiyo.

Wachambuzi wa siasa nchini Kenya wanaona itakuwa ni kazi ngumu kwa viongozi hao wa Kenya kuhudhuria vikao vya ICC wakati uo huo wakihitajika kuongoza nchi.

Wataalam wa Mahakama ya ICC wanasema kuwa ikiwa wawili hao hawatashirikiana na Mahakama hiyo huenda wakawekewa agizo la kukamatwa kama ilivyokuwa kwa rais wa Sudan Omar Al Bashir.

Kesi ya Uhuru inatarajiwa kuanza mwezi wa Julai huku ile ya Ruto ikianza mwezi wa Mei mwaka huu.