DRC-M23

Waasi wa M 23 wasema jeshi la UN kuamua mustakabali wa amani Mashariki mwa DRC

Waasi wa M 23 Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanasema hatua ya Umoja wa Mataifa kutuma jeshi lake kukabiliana nao itaamua mustkabali wa amani katika eneo hilo.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa jeshi la M 23 Vianney Kazarama amesema kuwa jeshi hilo litalipa kundi hilo ushindi au uongozi wa rais Joseph Kabila, uongozi ambao kundi hilo linaona kuwa chanzo kikubwa cha ukosefu wa usalama Mashariki mwa nchi hiyo.

Kundi hilo lisema kuwa ikiwa litashambuliwa, halitakuwa na njia nyingine ila kupigana na jeshi hilo la Umoja wa Mataifa hali ambayo wachambuzi wa siasa na usalama nchini DRC wanaona kuwa huenda ikasababisha hali kuwa mbaya zaidi katika eneo hilo.

Rwanda ambayo inashukiwa na Umoja wa Mataifa kuwasaidia waasi hao wa M23 imelaani hatua ya Umoja wa Mataifa kutuma wanajeshi wake Mashariki mwa DRC, inasema suluhu la kupata amani Mashariki mwa nchi hiyo ni la kisiasa wala sio kupeleka wanajeshi.

Wakati hayo yakijiri, mazungumzo ya amani kati ya kundi hilo na wajumbe wa serikali wa Kinsasha yanaendelea jijini Kampala Uganda na hadi sasa haijafamika ni lini yatafikia mwisho na kutiwa saini.

Kwingineko, Mahakama moja katika mji wa Bandundu Magharibi mwa nchi hiyo imewahukumu jela wanaharakati 12 wa haki za binadamu miaka 20 jela baada ya kubainika kushirikiana na makundi ya waasi.