KENYA

Wabunge nchini Kenya wasema wataendelea kupigania nyongeza ya mishahara yao

Wabunge nchini Kenya wanasema wataendelea kuishinikiza tume inayoshughulikia mishahara ya watumishi wa umma kuwaongezea mshahara wao  baada ya kuupunguza.

Matangazo ya kibiashara

Matumaini ya wabunge hao kuongezewa mishahara hata hivyo yalionekana kudidimia siku ya Jumanne wakati rais Uhuru Kenyatta alipofungua bunge na kusema hakuna mabadiliko yatakayofanywa kuhusu mishahara mipya iliyowekwa na tume hiyo.

Aidha, rais Kenyatta alisema ni jukumu la wabunge nchini humo kuhakikisha kuwa kuna utumizi mzuri wa fedha za umma ili kuepuka mgogoro wa kiuchumi nchini humo kwa sababu ya mishahara mikubwa.

Tume inayoshughulikia mishahara nchini humo ilipunguza mshahara wa wabunge hao kutoka Dola 10,000 hadi Dola 5,955 kwa wabunge wote wapya wa bunge la kumi na moja hatua ambayo imewakasirisha wabunge hao.

Kabla ya kupunguzwa kwa mishahara hiyo, wabunge nchini humo walikuwa ndio wanaolipwa mshahara kubwa zaidi katika nchi za Jumuiya Madola kote duniani.

Tume ya kushughulikia mishahara ya watumishi wa Umma ikiongozwa na Sarah Serem inasema ilichukua hatua hiyo ili kuweka usawa wa malipo kwa wafanyikazi wote wa serikali nchini humo.

Hata hivyo, tume hiyo imeshtumiwa kuwaongezea wenyeviti wa Kamati mbalimbali kama ile ya utekelezaji wa katiba kupata mshahara mkubwa kwa kile wanachokisema hawana kazi nyingi ya kufanya.

Wabunge nchini humo katika miaka iliyopita wamekuwa wakijiongezea mishahara na sasa wanasema hawawezi kutekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwa mshahara wao hautaongezwa.