SUDAN

Wanajeshi saba wa Sudan waliohukumiwa jela kwa jaribio la kuipindua serikali ya Bashir waachiliwa huru

Wanajeshi saba nchini Sudan waliohukumiwa jela miaka mitano kwa kupanga jaribio za kumpindua kijeshi rais Omar Al Bashir wameachiliwa huru siku chache baada ya kuhukumiwa jela.

Matangazo ya kibiashara

Miongoni mwa wanajeshi hao ni Brigedia Mohammed Ibrahim, ambao baada ya kuachiliwa huru wamepata makaribisho makubwa kutoka kwa familia zao na wafuasi wao jijini Khartoum.

Haijafamika vema ni kwanini wanajeshi hao waliachiliwa huru lakini walimwomba rais kuwaachilia .

Wachambuzi wa siasa nchini Sudan wanasema kuwa ikiwa wanajeshi hao wangeendelea kuwa uongozini huenda wangenyongwa kutokana na hatua hiyo ambayo ingesababisha machafuko ya kisiasa nchini humo.

Mapema mwezi huu rais Bashir alitangaza kutoa msamaha kwa wafungwa wote wa kisiasa suala ambalo wachambuzi wa siasa za Sudan  wanaona kuwa huenda imechangia kuachiliwa huru kwa wafungwa hao.

Sudan iko katika harakati za kupata katiba mpya na kuimarisha taasisi mbalimbali na tayari rais Bashir amesema kuwa hatawania tena urais nchini humo.

Rais Bashir anatakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya ICC kutokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyotokea katika Jimbo la Darfur kati ya mwaka 2003 hadi 2010.

Mataifa hisani mwezi huu yalikutana mjini Doha nchini Qatar kukusanya fedha za kulijenga upya jimbo la Darfur.