AFRIKA KUSINI-M 23

Afrika Kusini yataja kikosi kitakachopambana na waasi wa M 23 Mashariki mwa DRC

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ametangaza kuwa wanajeshi 1,345 wa nchi hiyo watajumuishwa katika kikosi cha Umoja wa Mataifa kitachokwenda Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kukabiliana na waasi wa M 23 na makundi mengine ya uasi.

Matangazo ya kibiashara

Tangazo hili limetolewa na rais Zuma wiki chache tu  baada ya wanajeshi 13 wa nchi hiyo kuuawa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wakati wa makabiliano kati ya waasi wa Seleka na wanajeshi wa serikali.

Rais Zuma amesema kuwa tayari bunge nchini humo limeshafahamishwa kuhusu Oparesheni hiyo mpya huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Afrika Kusini inasema kuwa wanajeshi wake watakaokwenda nchini DRC wana uzoefu mkubwa wa kulinda amani katika mataifa mbalimbali duniani  na hawatishwi na waasi wa M 23.

Wanajeshi wa Afrika Kusini wataungana pamoja na wenzao kutoka Tanzania na Malawi kukabiliana na waasi hao wa M 23 ambao wameonya kuwa ikiwa watashambuliwa watakabiliana na vikosi hivyo vya Umoja wa Mataifa.

Mwezi uliopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuwatuma wanajeshi 19,815 kusaka silaha kutoka kwa makundi ya waasi na kulinda amani ikiwa ni pamoja na kupambana na waasi hao ikiwa vita vitazuka.

Wakati hayo yakijiri, mazungumzo ya amani kati ya kundi hilo na wajumbe wa serikali wa Kinsasha yanaendelea jijini Kampala Uganda na hadi sasa haijafamika ni lini yatafikia mwisho na kutiwa saini.