JAMHURI YA AFRIKA YA KATI-CHAD

Mkutano wa kuisaidia Jamhuri ya Afria ya Kati wafanyika nchini Chad

Viongozi wa mataifa ya Jumuiya ya Afrika ya Kati wanakutana mjini Djamena nchini Chad kujadiliana kuhusu hatima ya kisiasa na usalama nchini Jamhuri ya Afrika ya  Kati.

Matangazo ya kibiashara

Miongoni mwa maswala nyeti yanayojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na namna ya kuisaidia nchi hiyo kuimarisha usalama pamoja na kuweka uthabiti wa kisiasa baada ya mapinduzi kutokea mwezi uliopita.

Kabla ya mkutano huo serikali hiyo ya Jamhuri ya Afrika ya Kati iliomba Ufaransa na mataifa yake jirani kuisaidia kijeshi na kifedha ili kuirejea katika hali yake ya kawaida baada ya kutokea kwa mapinduzi hayo.

Waziri Mkuu Nicolas Tiangaye amesema nchi yake inahitaji msaada huo ili kusonga mbele kiuchumi, kiusalama na kisiasa hasa kutokana na machafuko ambayo yameendelea kushuhudiwa jijini Bangui ambayo mwishoni mwa wiki iliyopita watu 20 waliuawa katika makabiliano kati ya maafisa wa usalama na raia.

Tiangaye amesema raia wengi katika jiji la Bangui wanapitia hali ngumu na wengi wao wametorokea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kama wakimbizi wakiwemo watoto.

Rais wa Mpito  Michel Djotodia, ambaye aliongoza kundi la Seleka kutekeleza mapinduzi hayo dhidi ya uongozi wa rais Francos Bozize ameahidi kuimarisha usalama jijini Bangui kwa kuongeza idadi ya polisi wanaotoa usalama kwa wakaazi wa jiji hilo.