NIGERIA

Serikali ya Nigeria yaunda Kamati maalum kuhusu kundi la Boko Haram

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ameunda Kamati maalum ya kujaribu kutekeleza hatua ya kutoa msamaha kwa wanachama wa kundi la kiislamu la Boko Haram.

Matangazo ya kibiashara

Kamati hiyo itakutana kwa siku 60 zijazo kujaribu kuzungumza na Boko Haram na kuwapokonya silaha ambazo zinasalia kuhatarisha usalama kwa rais wa nchi hiyo.

Aidha, kamati hiyo itaweka mikakati ya kuwasaidia wahanga wote walioathiriwa na mashambulizi kutoka kwa kundi hilo.

Boko Haram imekuwa ikifanya mashambulizi hasa Kaksazini mwa nchi hiyo kuanza mwaka 2009 na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha yao.

Kamati hiyo ina wanachama 25 wakiwemo viongozi wa kijeshi, wanasiasa na wasomi ambao wana jukumu la kuchunguza kiini cha mashambulizi hayo na kupendekeza mbinu za kulitokomeza kabisa kundi hilo la Boko Haram.

Wakati uo huo, serikali ya Nigria imebuni Kamati nyingine ya kushughulikia maswala ya usalama nchini humo na kutafuta suluhu ndogondogo ili kuimarisha usalama nchini humo.

Kamati hizo zinatarajiwa kuanza kazi rasmi tarehe 24 mwezi huu.

Rais Jonathan amekuwa akipokea shinikizo kutoka kwa viongozi wa kisiasa kutoka Kaskazini mwa nchi hiyo akiwemo Sultan wa jimbo la Sokoto kutoa msamaha kwa Boko Haram ili kundi hilo kuachana na mashambulizi yake.

Hata hivyo, wachambuzi wa siasa nchini humo wanasema kuwa haitakuwa rahisi kwa kamati hiyo kufanya mazungumzo na kundi hilo baada ya wanamgambo hao kusema kuwa hawataki kuzungumza na serikali.