ZIMBABWE

Mugabe ataka mataifa ya Magharibi kutoingilia Uchaguzi Mkuu nchini mwake

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amesema hatakubali mataifa ya Magharibi kuingilia Uchaguzi Mkuu nchini humo unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo, rais Mugabe amesema anakaribisha uamuzi wa mataifa hayo ya Magharibi ikiongozwa na Uingereza  kuwa tayari kushirikiana na nchi hiyo tena baada ya kuitenga kwa kipindi kirefu.

Akiwahotubia wananchi wa taifa hilo wakati wa kuadhimisha miaka 33 ya Uhuru wa taifa hilo, rais Mugabe amesema Zimbabwe imekuwa ikitengwa kwa tuhma za kutoendesha uchaguzi wa huru na haki na maswala ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Rais huyo mkongwe  barani Afrika amesisitiza kuwa wakati umefika kwa viongozi wa nchi za Magharibi kuwaacha waafrika kufanya uamuzi wao wenyewe ikiwemo kuwachagua viongozi wanaowataka.

Uchaguzi nchini Zimbwabe huenda ukafanyika kati ya mwezi wa Juni na Septemba na rais Mugabe ametoa wito kwa wananchi wa taifa hilo kushiriki kwenye uchaguzi huo kwa amani.

Naye Waziri Mkuu Morgan Tsangirai katika ujumbe wake alisema uhuru waliopata kutoka kwa Uingereza bado haujaonekana kwa raia wa kawaida nchini humo kutokana na kutokuwa na uhuru wa kujieleza, na haki zingine za msingi.

Rais Mugabe na Waziri Mkuu Tsangirai wanaongoza serikali ya muungano nchini baada ya machafuko ya baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2008.