JAMHURI YA AFRIKA YA KATI-CHAD

Muungano wa nchi za Afrika ya Kati waitambua serikali ya rais Michel Djotodia

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika ya Kati ECCAS wameitambua serikali ya mpito ya rais Michel Djotodia nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano wa viongozi hao kutoka Gabon, Cameroon, Congo na wenyeji wa mkutano huo Chad walikutana mjini Djamena kuzungumzia hali ya kisiasa na usalama nchini humo baada ya mapinduzi ya waasi kutokea nchini humo mwezi uliopita na kuwepo kwa serikali ya mpito.

Aidha, viongozi hao wa ECCAS wamesema kuwa Jumuiya hiyo itatuma wanajeshi 2,000 kuimarisha usalama nchini humo baada ya waasi wa Seleka kukabiliana na wakaazi wa mji wa Bangui wakati wa zoezi la kuwapokonya silaha mwishoni mwa wiki iliyopita.

Jeshi hilo litasaidiana na wale wa serikali ya mpito kuimarisha usalama kwa serikali lakini haijafahamika ni lini litaanza oparesheni hiyo kusaidiana na wanajeshi wengine 500 kutoka mataifa mengine barani Afrika.

Suala la kuisaidia Jamhuri ya Afrika ya Kati kifedha pia lilijadiliwa katika kikao hicho kutokana na hali ngumu ya kiuchumi inayoshuhudiwa na serikali hiyo ya mpito kwa sasa.

Wito kama huo wa fedha na jeshi ulitolewa na serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kupitia kwa Waziri Mkuu Nicolas Tiangaye kwa nchi ya Ufaransa na mataifa mengine barani Afrika  kuisaidia.

Wafuasi wa rais wa zamani aliyeondolewa madarakani kwa nguvu na waasi wa Seleka Francois Bozize wametoa wito kwa Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Kimataifa kutoitambua serikali ya mpito nchini humo wanayosema ni ya majambazi.