COTE D'IVOIRE

Cote d'Ivoire yasubiri matokeo ya uchaguzi wa siku ya jumapili

REUTERS/Thierry Gouegnon

Tume ya uchaguzi nchini Cote D'Ivoire CEI inatarajiwa kutangaza matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa na Magavana uliofanyika siku ya jumapili huku wapiga kura wachache wakijitokeza kutokana na vyama vya upinzani kususia zoezi hilo.

Matangazo ya kibiashara

Chama kilichokuwa kinaongozwa na Rais wa zamani wa nchi hiyo Laurent Gbagbo ni miongoni mwa vyama vilivyosusia uchaguzi huo.

Mara baada ya kupiga kura yake Rais Alassane Ouattara alionekana mwenye kujiamini huku akiamini wananchi wengi wangejitokeza kushiriki kwenye kinyang'anyiro hicho.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Yusuf Bakayoko amekiri wapiga kura walikuwa wachache licha ya dosari chache kujitokeza kwani katika baadhi ya maeneo zoezi la upigaji kura liliuchelewa kutokana na kucheleweshwa kwa vifaa vya kupigia kura.

Kususiwa kwa uchaguzi huo wa serikali za mitaa kumeanza kuzua maswali mengi juu ya uongozi wa Rais Ouattara kutokana na wengi kuamini huenda akakumbana na upinzani mkubwa katika shughuli zake.

Umoja wa mataifa UN umelitaka Taifa hilo kuwa na utulivu ili kuepuka kutonesha majeraha ya ghasia zilizozuka baada ya uchaguzi uliopita wa mwaka 2010 baada ya Gbagbo kupinga matokeo na kusababisha kuzuka kwa machafuko.